Deuteronomy 28

Baraka Za Utiifu

(Walawi 26:3-13; Kumbukumbu 7:12-24)

1 aKama ukimtii Bwana Mwenyezi Mungu wako kwa bidii na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa bidii, Bwana Mwenyezi Mungu wako atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. 2 bBaraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Bwana Mwenyezi Mungu wako:

3 cUtabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.

4 dUtabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na wanyama wako wachanga wa kufugwa, yaani ndama wa makundi yako ya ng’ombe, na wana-kondoo wa makundi yako.

5Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.

6

eUtabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.

7 f Bwana atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.

8 g Bwana ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Bwana Mwenyezi Mungu wako atakubariki katika nchi anayokupa.

9 h Bwana atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, kama ukishika maagizo ya Bwana Mwenyezi Mungu wako na kwenda katika njia zake. 10 iKisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Bwana, nao watakuogopa. 11 j Bwana atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwapa.

12 k Bwana atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote. 13 l Bwana atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Bwana Mwenyezi Mungu wako ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa bidii, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini. 14 mUsihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.

Laana Kwa Kutokutii

(Walawi 26:14-46)

15 nHata hivyo, kama hutamtii Bwana Mwenyezi Mungu wako na kuzishika kwa bidii amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata:

16Utalaaniwa mjini na utalaaniwa mashambani.

17Kapu lako na chombo chako cha kukandia kitalaaniwa.

18 oUzao wa tumbo lako utalaaniwa, mazao ya ardhi yako, ndama wa makundi yako ya ng’ombe na wana-kondoo wa makundi yako.

19

Utalaaniwa uingiapo na utokapo.

20 p Bwana ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, mpaka uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye. 21 q Bwana atakupiga kwa magonjwa mpaka akuangamize kutoka nchi unayoingia kuimiliki. 22 r Bwana atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga mpaka uangamie.

23 sAnga juu yako itakuwa shaba, na ardhi chini yako itakuwa chuma. 24 t Bwana atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga; vitakujia kutoka angani mpaka uangamie.

25 u Bwana atakufanya ushindwe mbele ya adui zako. Utawajia kwa njia moja lakini utawakimbia mbele yao kwa njia saba, nawe utakuwa kitu cha kuchukiza kwa falme zote za dunia. 26 vMizoga yenu itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwepo mtu yeyote wa kuwafukuza. 27 w Bwana atakupiga kwa majipu ya Misri na kwa vidonda vitokavyo usaha na kuwashwa, ambako huwezi kuponywa. 28Bwana atakupiga kwa wazimu, upofu na kuchanganyikiwa kwa akili. 29 xWakati wa adhuhuri utapapasapapasa huku na huko kama mtu kipofu katika giza. Hutafanikiwa katika lolote ufanyalo; siku baada ya siku utaonewa na kunyang’anywa, wala hakuna yeyote atakayekuokoa.

30 yUtaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake. 31Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu yeyote wa kuwaokoa. 32Wanao na binti zako watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono. 33 zTaifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote. 34Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu. 35 aa Bwana atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.

36 ab Bwana atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe. 37 acUtakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Bwana atakakokupeleka.

38 adUtapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila. 39 aeUtapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila. 40 afUtakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika. 41Utakuwa na wana na binti lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka. 42 agMakundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.

43Mgeni anayeishi miongoni mwako atainuka juu zaidi na zaidi kuliko wewe, lakini wewe utashuka chini zaidi na zaidi. 44 ahYeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.

45 aiLaana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata mpaka uangamizwe, kwa sababu hukumtii Bwana Mwenyezi Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa. 46 ajZitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele. 47 akKwa sababu hukumtumikia Bwana Mwenyezi Mungu wako kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako, 48 alkwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Bwana atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.

49 am Bwana ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukiavyo mawindo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake, 50 antaifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana. 51 ao apWatakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako mpaka umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako mpaka umekuwa magofu. 52 aqNao wataizingira miji yote katika nchi yako mpaka kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Bwana Mwenyezi Mungu wako anakupa.

53 arUtakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako na binti zako ambao Bwana Mwenyezi Mungu wako amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira. 54Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia, 55 asnaye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote. 56 atMwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake, 57 aukondoo wa nyuma kutoka kwenye tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile ambazo adui yako atazileta juu yako na miji yako.

58 avKama hutafuata kwa bidii maneno yote ya sheria hii, ambayo yameandikwa katika kitabu hiki na kama hutalicha hili jina la fahari na la kutisha, yaani la Bwana Mwenyezi Mungu wako, 59 aw Bwana ataleta mapigo ya kutisha juu yako na kwa wazao wako, maafa makali na ya kudumu, magonjwa mazito na ya kudumu. 60 axAtakuletea juu yako magonjwa yote ya Misri yale uliyoyaogopa, nayo yataambatana nawe. 61 ayPia Bwana atakuletea kila aina ya ugonjwa na maafa ambayo hayakuandikwa humu katika kitabu hiki cha sheria, mpaka utakapokuwa umeangamizwa. 62 azNinyi ambao mlikuwa wengi kama nyota za angani mtaachwa wachache tu, kwa sababu hamkumtii Bwana Mwenyezi Mungu wenu. 63 baKama ilivyompendeza Bwana kuwafanya ninyi mstawi na kuongezeka kwa idadi, ndivyo itakavyompendeza kuwaharibu na kuwaangamiza ninyi. Mtang’olewa kutoka nchi mnayoiingia kuimiliki.

64 bbKisha Bwana atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwingine. Huko mtaabudu miungu mingine, miungu ya miti na ya mawe, ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua. 65 bcMiongoni mwa mataifa hayo hamtapata raha wala mahali pa kupumzisha wayo wa mguu wenu. Huko Bwana atawapa mahangaiko ya mawazo, macho yaliyochoka kwa kungojea na moyo uliokata tamaa. 66Utaishi katika mahangaiko siku zote, ukiwa umejaa hofu usiku na mchana, wala hutakuwa kamwe na uhakika wa maisha yako. 67 bdWakati wa asubuhi utasema hivi, “Laiti ingekuwa jioni!” Jioni utasema, “Laiti ingekuwa asubuhi,” kwa sababu ya hofu ile itakayojaza moyo wako na vitu vile macho yako yatakavyoviona. 68 be Bwana atawarudisha tena Misri kwa meli, safari niliyosema kamwe hamngeenda tena. Huko mtajiuza ninyi wenyewe kwa adui zenu kama watumwa wa kiume na wa kike, lakini hakuna yeyote atakayewanunua.
Copyright information for SwhKC